Elimu ya jadi: ina umuhimu au ni ya
‘ki-shenzi’
Na David Simiyu.
Wakoloni
walipokuja Afrika walikuta wenyeji wakiwa na mifumo yao ya elimu. Wenyeji
walikua na namna yao ya kutatua matatizo ya kiafya, kisheria, kimazingira, hali
ya hewa na kadharika. Kwa bahati mbaya wakoloni walifanya kila wawezalo ili
kuondoa mifumo ya kijadi na kuiita kuwa ni ya kishenzi.
Baraza
la kimataifa la sayansi (the international council for science-ICSU)
linaitambua elimu ya jadi na linaielezea elimu ya jadi kuwa ni “Ufahamu na
ujuzi ulioendelezwa na watu baada ya miaka mingi ya muingiliano baina yao na
mazingira asili” (ICSU, 2012). Elimu ya aina hii hurithishwa kutoka kizazi na
kizazi kupitia njia za kitamaduni kama vile nyimbo, hadithi, misemo, methali,
miiko, jando na unyago.
Kabla
ya ujio wa mfumo wa elimu unaotumika sasa, ambapo vijana hukaa darasani na
kufunzwa kuhusu mambo mbalimbali kama vile Sanaa, michezo, sayansi, lugha na
kadhalika, jamii nyingi zilikuwa na mifumo yao ya elimu. Jamii zetu zilikuwa na
njia zao za kukabili changamoto mbalimbali zilizowakabili. Kulikuwa na mifumo
na jinsi za kukabiliana na majanga ya kimazingira, magonjwa, masuala ya sharia
na maamuzi, na mambo mengine mengi yaliyozikabili jamii zetu. Na njia hizi
ndizo zilizofanya jamii hizi zikawa na ustawi, ni ufahamu wao ndio
uliowawezesha kukabili changamoto hizi, na ufahamu huu (ambao ndiyo kinachoitwa
elimu ya jadi) ulirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Kukosekana
kwa namna bora ya kuhifadhi elimu hii ya jadi pamoja na ujio wa mifumo ya elimu
na kitamaduni ya kigeni, zimesababisha kumomonyoka kwa mifumo ya elimu ya jadi.
Lakini je, ni hiki pekee kinachosababisha kuanguka kwa mifumo ya elimu ya jadi?
Baadhi ya watu wamediriki kuiita mifumo ya elimu ya jadi kama ya “kishenzi” na
isiyo na nafasi katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia. Kwa bahati mbaya
wametufanya hata sisi tuliokuwa tunaimiliki mifumo hii katika tamaduni zetu
kuamini hivyo. Lakini kuna baadhi ya watu bado wana imani kubwa juu ya elimu
hii ya jadi, wanatetea mifumo yake na wanatoa hoja kuwa elimu hii ina misingi
ya sayansi ndani yake. Wanachopendekeza watetezi wa elimu ya jadi sio kuiacha
elimu ya kisasa, bali kuwe na mfumo utakao ziunganisha aina zote mbili, na kwa
maoni yao ni kuwa hii ndiyo njia pekee ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii
zetu hasa katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazotukabili.
Je,
ni kweli elimu ya jadi inamisingi ya
kisayansi?
Ili
kufahamu kama elimu ya jadi ni sayansi, inabidi kwanza tuelewe nini maana ya
sayansi. Wanazuoni wengi wametoa maana zao juu ya dhana ya sayansi, mmoja wao
ni Wilson O. Edward, ambaye alisema kuwa,
“sayansi
ni mfumo ulio pangika ambao hutumika kukusanya taarifa kuhusu mambo mbalimbali
na kupanga taarifa hizi katika sheria na taratibu zinazoweza kujaribiwa na
kuthibitishwa” (tafsiri yangu mwenyewe kutoka kwa Wilson 1998).
Kutoka
katika maana hiyo ya sayansi, Wilson anatanabaisha sifa mbili kuu za sayansi,
kuwa ni uwezo wa kurudiwa na watu wengine na kutoa matokeo yaleyale na sifa ya
pili kuwa ni uwezo wa kuchagiza uvumbuzi (heuristic).
Je, elimu ya jadi inaingia katika maana ya sayansi iliyotajwa hapo juu?
Kwanza
tukumbuke kuwa, elimu ya jadi ni matokeo ya uzoefu wa watu uliokusanywa na kuwa
ufahamu baada ya miaka mingi ya kuingiliana na mazingira yao. Kama ilivyo
mifumo mingine ya kisayansi, elimu ya jadi inafuata taratibu ambazo zinaweza
kurudiwa na mtu mwingine yeyote na kutoa matokeo yanayofanana. Tukichukua mfano
wa mganga wa jadi, yeye hufahamu mmea mahsusi unaohusika kutibu ugonjwa
mahsusi, hufahamu kwa ufasaha ni sehemu gani ya mmea huo utumike, hufahamu pia
hatua za kuandaa tiba husika, na pia hata jinsi ya kumpatia mgonjwa hiyo dawa
(kwa kuchanja mwili, kunywa na maji, kunusa, kufukiza n.k). ukichunguza kwa
umakini mlolongo huu, utagundua kuna aina fulani ya mtiririko maalumu ambao
lazima ufuate katika kuandaa mmea fulani kuwa tiba ya ugonjwa fulani.
Ni
kweli kuwa, kuna baadhi ya mambo katika elimu ya jadi ambayo ukiyatazama kwa
mtizamo kwa sayansi ya kimagharibi itaonekana kama haiendani kabisa na misingi
ya sayansi. Kwa mfano, katika chapisho la Sunseri (2003), kumetajwa baadhi ya
Imani kutoka katika kabila la wazaramo wa Tanzania ambao huamini kuwepo kwa
mizimu katika miti mikubwa ndani ya misitu yao. Imani kama hii ni kweli haiwezi
kujaribiwa na kuthibitishwa kisayansi, lakini hebu jaribu kufikiria matokeo ya
Imani kama hii katika kufanikisha uhifadhi wa uoto wa asili na mazingira kwa ujumla.
Imani kama hizi, ziliendana na zuio la kuingia katika baadhi ya misitu na pia
ukataji wa miti ndani ya misitu. Na hata inapobidi ukataji wa miti kufanyika
kwa ajili ya ujenzi na shughuri nyingine kulikuwa na taratibu za kufuatwa za
kijadi ili kuingia msituni na kukata miti iliyoelekezwa.
Kwa
nini basi watu wa asili walitoa hadhi ya mizimu na matambiko kwa miti na mimea
maalum? Miti na mimea hii (na hata baadhi ya wanyama), ilipewa hadhi hii ili kuweza
kupata hadhi maalumu ya kuhifadhiwa. Katika sayansi ya kimagharibi, mimea ya
aina hii inaweza kuitwa mimea iliyo katika hatari ya kutoweka “threatened”.
Haiingii akilini kwa jamii hizi kuipa hadhi ya mizimu mimea ambayo ipo kwa
wingi katika msitu, mara nyingi heshima hii ilipewa miti ambayo ni michache sana
katika msitu.
Kwa
maana hiyo, pamoja na kuwa Imani kama hizi zinaonekana hazina usayansi ndani
yake, lakini ni ukweli kuwa sababu zake zinamisingi ya sayansi ya uhifadhi. Na
ndio maana, kabla ya ujio wa wakoloni na mifumo yao ya elimu na kuiita mifumo
yetu ya elimu kuwa ni ya kishenzi na isiyo ya kisayansi, uharibifu wa mazingira
unaosababishwa na shughuri za kibinadamu haukuwepo.
Tofauti
ni ipi kati ya sayansi ya kijadi na ile ya kisasa?
Utofauti
mkubwa ambao nauona kati ya mifumo hii miwili ni kuwa, katika sayansi ya
kijadi, vitu ambavyo havieleweki kwa akili ya kibinadamu vilikuwa na njia
maalum ya kuvishughurikia, na hii ni katika lengo moja mahsusi la kuiacha asili
ijihifadhi yenyewe. Hii ni kwa maana kwamba, kuviingilia vitu visivyofahamika
kiundani ni kujaribu kuvitibua asili yake na hivyo kusababisha madhara hasi kwa
asili yenyewe na hata jamii inayoizunguka. Vitu hivi visivyofahamika vyema hata
kwenye sayansi ya kisasa vipo vingi tu, na kiukweli baadhi ya dhana za
kisayansi zimekuwa zinakanushwa mara kwa mara. Kwa mfano dhana kuu kuhusu
“urithi wa geni” ijulikanayo kama “the
central dogma” ambapo ilidhaniwa kuwa jeni moja hutengeneza protini moja,
imekwisha kuthibitishwa kuwa siyo kweli (Waynne 2007).
Sayansi
ya jadi inayachukulia mambo yote yasiyofahamika vyema katika mtazamo kuwa
ulimwengu umeumbwa katika uwiano fulani na kwamba shughuri za binadamu
zinatakiwa zisitibue uwiano huu wa asili. Hivyo basi jamii za kijadi zimekuwa
na taasisi maalumu (kama vile wazee, waganga wa jadi au watabiri) zenye kutoa
muongozo wa jinsi ya kushughurika na mambo yasiyofahamika vyema. Kwa sayansi ya
kisasa mambo yote yasiyoelezeka na kufahamika vyema yanafaa kuchunguzwa hadi yafahamike
vyema bila kujali madhara yake. Sayansi hii imejikita katika kufanya majaribio
hata kama matokeo ya majaribio hayo hayafahamiki vyema. Kwa hali ilivyofikia
sasa, tafiti za kisayansi hazifanyiki tu ili kutazama na kutaka kufahamu
kinachotokea katika mambo mbalimbali bali kujaribu kubadili ufanyaji kazi wa
mambo mbalimbali kama seli za uhai ili tu kuona jambo litakalotokea.
Chanzo
kikuu cha elimu ya jadi ni mazingira yanoyozunguka jamii husika. Na ndio mimea
inayopewa hadhi ya uhifadhi katika jamii ya watu wa Ruvuma inaweza kuwa tofauti
na mimea inayopewa hadhi maalum na watu wa Pwani. Hii ni kwa sababu jamii hizi
zinazungukwa na mazingira tofauti. Jambo la kutilia maanani ni kuwa,
uhusishwaji wa elimu hii ya jadi na utamaduni pamoja na Imani za jamii fulani,
isitumike kama kigezo cha kufifisha umuhimu wa elimu hii hasa katika mazingira
ya sasa ya uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na shughuri mbalimbali
za kibinadamu, magonjwa mengi, mabadiliko ya tabia nchi na hata upungufu wa
chakula.
elimu ya jadi humfunganisha mtu na mazingira yake.
Tunawezaje kuitumia elimu ya jadi
katika zama hizi za sayansi na teknolojia?
Jinsi
watu wa asili walivyojifunza elimu yao inatoa mwanga wa umuhimu wa elimu hii. Elimu
hii haikupatikana kwa njia moja tu ya kushibisha akili, elimu hii iligusa
sehemu kuu nne za maisha ya mtu. Iligusa akili, iligusa pia hisia, roho (imani)
na pia nguvu za kimwili (utendaji). Kama tutaweza kuihusisha aina hii ya elimu
katika mfumo wetu rasmi wa elimu ya kisasa, itaongeza sana ubora hasa katika
kipengele cha ufanisi wa watu wanaohitimu mafunzo katika kukabili changamoto mbalimbali
za maisha.
Kati
ya tabia kuu za elimu ya jadi ni kusisitiza uwajibikaji wa kijumla. Hii ni
kuhimiza ushirikiano wa jamii nzima katika kuheshimu ardhi na mazingira,
kuheshimu pia uwiano na utegemeanaji wa viumbe na pia umuhimu wa kutumia tu
kile kinachohitajika. Ingawa Tanzania ni moja kati ya nchi zinazoongoza katika
kutenga ardhi kwa ajili ya uhifadhi (kwa takwimu za 2011 za shirika la
maendeleo la umoja wa mataifa, kilometa za eneo takribani 250,000 za ardhi yote
imetengwa kwa ajili ya uhifadhi ambayo ni takribani 27%, ikijumuisha mapori ya
hifadhi, mbuga za wanyama n.k), lakini ni moja kati ya nchi zinazokabiliwa na
upotevu mkubwa wa maliasili (aina za mimea takribani 240 ipo katika hatari ya
kutoweka kati ya aina za mimea takribani 10,000 inayopatikana Tanzania, wanyama
(mamalia) 42 kati ya 316, na ndege 33 kati ya 229).
Kasi hii ya upotevu wa
maliasili inaweza kuhusishwa kwa kiasi fulani na kushindwa kwa elimu ya
uhifadhi ya kimagharibi ambayo inatolewa kwa jamii ambazo tayari zilikuwa na
mifumo yao thabiti ya uhifadhi iliyokuwa inatolewa na elimu yao ya jadi. Hebu tazama
tu katika jamii tunayoishi sasa jinsi ambavyo chochote ambacho ni cha uma
kinavyo chukuliwa. Wala tusishangae jinsi jamii hizi zinavyoshindwa kujali
mazingira na kupelekea madhara kama tuliyonayo sasa. Hivyo kuingiza katika
mitaala yetu jinsi nzuri ya uhifadhi shirikishi ni moja ya njia ya kuunganisha
elimu jadi nah ii ya kisasa.
Matumizi
ya elimu ya jadi katika elimu ya kisasa sio kitu kigeni duniani, na kwa hivyo
sio kazi ngumu kufanyika. Tukichukulia mifano iliyowazi katika nyanja ya
utengenezaji wa madawa, wanasayansi wa kimagharibi ambao hufanya kazi katika
makampuni makubwa ya utafiti na utengenezaji wa dawa za maradhi mbalimbali, hufanyia
kazi kwa ukaribu elimu ya jadi kutoka kwa wenyeji wa maeneo inakopatikana
misitu mbalimbali hasa Afrika, Asia na Amerika Kusini. Watu wanaoishi katika
maeneo inakopatikana misitu ya kitropiki wameweza kukusanya ujuzi na ufahamu mwingi
kuhusu matumizi ya mimea mbalimbali kama dawa. Hivyo basi kwa kutambua hilo,
makampuni ya dawa hukusanya taarifa hizi kutoka kwa wenyeji na kuzitumia katika
tafiti zao za dawa mbalimbali. Huu ni ushahidi tosha kwamba, hata leo, elimu ya
jadi inanafasi kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia yetu. Hili tunaweza
kulitanua kutoka katika tafiti za madawa hadi katika nyanja nyingine za elimu
tunayoitoa sasa.
Wenyeji wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na majanga ya kiasili mara kwa mara kama vile vimbunga na matetemeko ya ardhi, huwa na ujuzi wa kusoma tabia za wanyama mbalimbali kama mbwa, ndege na hata nyoka katika kutabiri ujio wa majanga hayo ya asili. Kukosa ufahamu wa kujua namna ambavyo wanyama hawa hujua kutabiri majanga na namna ambavyo watu huweza kuwasoma kwa usahihi, visizuie kuiingiza elimu hii na nyingine kama hizi katika mifumo rasmi ya ufundishaji mashuleni. Tutumie ujuzi na ufahamu wa jamii za kijadi katika kuingiza mafundisho
ya kinsi ya kufanya kilimo bora, ufugaji bora, elimu bora na hata utabibu. Tuache
kujaribu kuzi “staarabisha” jamii zetu za kijadi.
Pamoja
na yote ni lazima tukubali kwamba elimu ya kisasa inayo mazuri mengi lakini
tusizipuuze changamoto zake. Kwa mfano migogoro mbalimbali kati ya wakaazi wa
maeneo yanayozunguka hifadhi za kitaifa ambayo imeshapelekea madhara makubwa hata vifo,
migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya kisiasa n.k inachangiwa sana na
kujaribu kuleta majibu ya kisasa kwa changamoto za kijadi.
Yangu
ni hayo, tujitafakari na pia tusisahau kamwe kwamba “asili ni mali”.
David Simiyu
0764843000