Friday, 23 December 2016

INDIGENOUS PEOPLE'S BLOOD PATENTED. (matajiri wajimilikisha damu ya watu wa jamii za asili)




Wakati mwingine ni ngumu kuamini kwamba watu wa jamii fulani wanaweza kujimilikisha kisheria watu wa jamii nyingine. Ilitokea katika mkutano ule wa Berlin wakati wakoloni walipoligawana bara la Afrika na kujimilikisha kisheria kana kwamba nchi zetu zilikuwa bidhaa. Jambo hili tunaweza kudhani limekwisha baada ya nchi zetu kupata uhuru, lakini tunapaswa kujua bado hali hii inaendelea. Katika zama hizi ambapo haki za binadamu zinaongelewa kwa upana zaidi na kuwekwa katika katiba za nchi zote, mataifa makubwa na tajiri yanatumia silaha mpya inayoitwa “hakimiliki” (patent).
Mwaka 1994, serikali ya nchi tajiri ili katia hakimiliki damu ya watu wa jamii inayoishi katika visiwa vya bahari ya Pacific huko Papua New Guinea na visiwa vya Solomoni pamoja na watu wa jamii ya Guaymi kutoka Panama. Damu ya watu wa jamii hizi waligundulika kuwa na aina fulani ya virusi adimu viitwavyo T-Lymphotrophic Virus (HTLV). Virusi hivi vilikuwa ndo kwanza vinagundulika na hivyo kuvikatia hakimiliki vingeipa nchi hii fursa pekee ya kuvifanyia utafiti na hivyo kuweza kutengeneza kinga za magonjwa mbalimbali kupitia virusi hivi baada ya kuvihandisi.
Kwa maana nyingine, watu hawa walimilikishwa kisheria kabisa. Hawangekuwa na uwezo hata wa kuchukua vipimo vya damu zao wanapougua bila kwanza kuruhusiwa na nchi inayomiliki damu zao. Kwa bahati nzuri mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yalipigia kelele jambo hili na nchi hii ikaondoa hakimiliki yake kwa damu ya binadamu hawa.
Miaka sita iliyopita, shida hii ikawakuta watu wa jamii ya Baka, waishio katika mapori ya Cameroon. Kisa tu damu ya watu hawa iligundulika kuwa na aina mpya mbili za virusi vya HTLV (HTLV-3 na HTLV-4). Kwa kuwa kelele nyingi zilipigwa pale damu yote ya watu wa jamii zile za visiwa vya Pacific ilipo katiwa hakimiliki, kipindi hiki matajiri wakaamua kusema ‘tunajimilikisha tu virusi waliomo ndani ya damu za watu wa jamii ya Baka’.
Watoto wa kabila la Baka wakifurahi katika misitu wanayoishi huko Cameroon.
Leo hii hawana mamlaka na sehemu ya mwili wao. Wakiruhusu mtu mwingine awafanyie utafiti wanaweza hata kushtakiwa maana watakuwa wanachezea mali ambayo siyo yao kisheria. Na kinachouma zaidi ni kuwa, jamii ya watu hawa hawafaidiki chochote pamoja na kumilikishwa bila idhini yao. Bado wanaendelea kuishi katika mapori yao katika hali ambayo kwa tafsiri ya kimagharibi tutaita ni ya umasikini mkubwa.
Ni  kama vile watu weusi hawana kabisa haki dhidi ya asili yao. Nchi tajiri zimekuwa zikiendesha mipango yao kadhaa inayodhalilisha kabisa asili yetu. mifano ni mingi, na huenda ule uliotokea kwa watu masikini  weusi wa Alabama katika mwaka 1932 ndio umekua maarufu zaidi. Katika utafiti uliopewa jina la 'Tuskegee syphils experiment', wamarekani weusi waliambukizwa kwa makusudi (pasipo wao kufahamu), vimelea vya ugonjwa wa syphilis. Sio tu kwamba walipandikizwa ugonjwa, bali pia hawakupewa dawa ya ugonjwa huo ingawa dawa hiyo ilikwisha patikana katika kipindi cha utafiti huo. Hii ni moja kati ya kashfa kubwa ambayo ililikumba taifa la Marekani, na serikali hiyo haikuomba hata radhi kwa miongo kadhaa, hadi katika utawala wa  Bill Clinton (May 16, 2007) ndipo walau serikali iliomba radhi kwa kadhia hiyo.

Ni jukumu letu sote kulinda nchi zetu dhidi ya udhalilishaji. Tulinde asili tuliyopewa na Mungu, mambo mengine wala hayahitaji elimu kubwa kutambua uovu wake. Mwisho tusije kujikuta kila kilicho cha asili katika Afrika, sio chetu tena.

No comments:

Post a Comment