Sunday 1 January 2017

Elimu ya jadi (Indigenous knowledge), inaumuhimu au bado ni 'ya kishenzi'.



Elimu ya jadi: ina umuhimu au ni ya ‘ki-shenzi’
Na David Simiyu.

 
 
Wakoloni walipokuja Afrika walikuta wenyeji wakiwa na mifumo yao ya elimu. Wenyeji walikua na namna yao ya kutatua matatizo ya kiafya, kisheria, kimazingira, hali ya hewa na kadharika. Kwa bahati mbaya wakoloni walifanya kila wawezalo ili kuondoa mifumo ya kijadi na kuiita kuwa ni ya kishenzi. 

Baraza la kimataifa la sayansi (the international council for science-ICSU) linaitambua elimu ya jadi na linaielezea elimu ya jadi kuwa ni “Ufahamu na ujuzi ulioendelezwa na watu baada ya miaka mingi ya muingiliano baina yao na mazingira asili” (ICSU, 2012). Elimu ya aina hii hurithishwa kutoka kizazi na kizazi kupitia njia za kitamaduni kama vile nyimbo, hadithi, misemo, methali, miiko, jando na unyago.

Kabla ya ujio wa mfumo wa elimu unaotumika sasa, ambapo vijana hukaa darasani na kufunzwa kuhusu mambo mbalimbali kama vile Sanaa, michezo, sayansi, lugha na kadhalika, jamii nyingi zilikuwa na mifumo yao ya elimu. Jamii zetu zilikuwa na njia zao za kukabili changamoto mbalimbali zilizowakabili. Kulikuwa na mifumo na jinsi za kukabiliana na majanga ya kimazingira, magonjwa, masuala ya sharia na maamuzi, na mambo mengine mengi yaliyozikabili jamii zetu. Na njia hizi ndizo zilizofanya jamii hizi zikawa na ustawi, ni ufahamu wao ndio uliowawezesha kukabili changamoto hizi, na ufahamu huu (ambao ndiyo kinachoitwa elimu ya jadi) ulirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Kukosekana kwa namna bora ya kuhifadhi elimu hii ya jadi pamoja na ujio wa mifumo ya elimu na kitamaduni ya kigeni, zimesababisha kumomonyoka kwa mifumo ya elimu ya jadi. Lakini je, ni hiki pekee kinachosababisha kuanguka kwa mifumo ya elimu ya jadi? Baadhi ya watu wamediriki kuiita mifumo ya elimu ya jadi kama ya “kishenzi” na isiyo na nafasi katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia. Kwa bahati mbaya wametufanya hata sisi tuliokuwa tunaimiliki mifumo hii katika tamaduni zetu kuamini hivyo. Lakini kuna baadhi ya watu bado wana imani kubwa juu ya elimu hii ya jadi, wanatetea mifumo yake na wanatoa hoja kuwa elimu hii ina misingi ya sayansi ndani yake. Wanachopendekeza watetezi wa elimu ya jadi sio kuiacha elimu ya kisasa, bali kuwe na mfumo utakao ziunganisha aina zote mbili, na kwa maoni yao ni kuwa hii ndiyo njia pekee ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu hasa katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazotukabili.

Je, ni kweli elimu ya jadi  inamisingi ya kisayansi?
Ili kufahamu kama elimu ya jadi ni sayansi, inabidi kwanza tuelewe nini maana ya sayansi. Wanazuoni wengi wametoa maana zao juu ya dhana ya sayansi, mmoja wao ni Wilson O. Edward, ambaye alisema kuwa,
“sayansi ni mfumo ulio pangika ambao hutumika kukusanya taarifa kuhusu mambo mbalimbali na kupanga taarifa hizi katika sheria na taratibu zinazoweza kujaribiwa na kuthibitishwa” (tafsiri yangu mwenyewe kutoka kwa Wilson 1998).
Kutoka katika maana hiyo ya sayansi, Wilson anatanabaisha sifa mbili kuu za sayansi, kuwa ni uwezo wa kurudiwa na watu wengine na kutoa matokeo yaleyale na sifa ya pili kuwa ni uwezo wa kuchagiza uvumbuzi (heuristic).

Je, elimu ya jadi inaingia katika maana ya sayansi iliyotajwa hapo juu?
Kwanza tukumbuke kuwa, elimu ya jadi ni matokeo ya uzoefu wa watu uliokusanywa na kuwa ufahamu baada ya miaka mingi ya kuingiliana na mazingira yao. Kama ilivyo mifumo mingine ya kisayansi, elimu ya jadi inafuata taratibu ambazo zinaweza kurudiwa na mtu mwingine yeyote na kutoa matokeo yanayofanana. Tukichukua mfano wa mganga wa jadi, yeye hufahamu mmea mahsusi unaohusika kutibu ugonjwa mahsusi, hufahamu kwa ufasaha ni sehemu gani ya mmea huo utumike, hufahamu pia hatua za kuandaa tiba husika, na pia hata jinsi ya kumpatia mgonjwa hiyo dawa (kwa kuchanja mwili, kunywa na maji, kunusa, kufukiza n.k). ukichunguza kwa umakini mlolongo huu, utagundua kuna aina fulani ya mtiririko maalumu ambao lazima ufuate katika kuandaa mmea fulani kuwa tiba ya ugonjwa fulani.

Ni kweli kuwa, kuna baadhi ya mambo katika elimu ya jadi ambayo ukiyatazama kwa mtizamo kwa sayansi ya kimagharibi itaonekana kama haiendani kabisa na misingi ya sayansi. Kwa mfano, katika chapisho la Sunseri (2003), kumetajwa baadhi ya Imani kutoka katika kabila la wazaramo wa Tanzania ambao huamini kuwepo kwa mizimu katika miti mikubwa ndani ya misitu yao. Imani kama hii ni kweli haiwezi kujaribiwa na kuthibitishwa kisayansi, lakini hebu jaribu kufikiria matokeo ya Imani kama hii katika kufanikisha uhifadhi wa uoto wa asili na mazingira kwa ujumla. Imani kama hizi, ziliendana na zuio la kuingia katika baadhi ya misitu na pia ukataji wa miti ndani ya misitu. Na hata inapobidi ukataji wa miti kufanyika kwa ajili ya ujenzi na shughuri nyingine kulikuwa na taratibu za kufuatwa za kijadi ili kuingia msituni na kukata miti iliyoelekezwa.

Kwa nini basi watu wa asili walitoa hadhi ya mizimu na matambiko kwa miti na mimea maalum? Miti na mimea hii (na hata baadhi ya wanyama), ilipewa hadhi hii ili kuweza kupata hadhi maalumu ya kuhifadhiwa. Katika sayansi ya kimagharibi, mimea ya aina hii inaweza kuitwa mimea iliyo katika hatari ya kutoweka “threatened”. Haiingii akilini kwa jamii hizi kuipa hadhi ya mizimu mimea ambayo ipo kwa wingi katika msitu, mara nyingi heshima hii ilipewa miti ambayo ni michache sana katika msitu. 

Kwa maana hiyo, pamoja na kuwa Imani kama hizi zinaonekana hazina usayansi ndani yake, lakini ni ukweli kuwa sababu zake zinamisingi ya sayansi ya uhifadhi. Na ndio maana, kabla ya ujio wa wakoloni na mifumo yao ya elimu na kuiita mifumo yetu ya elimu kuwa ni ya kishenzi na isiyo ya kisayansi, uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuri za kibinadamu haukuwepo.

Tofauti ni ipi kati ya sayansi ya kijadi na ile ya kisasa?
Utofauti mkubwa ambao nauona kati ya mifumo hii miwili ni kuwa, katika sayansi ya kijadi, vitu ambavyo havieleweki kwa akili ya kibinadamu vilikuwa na njia maalum ya kuvishughurikia, na hii ni katika lengo moja mahsusi la kuiacha asili ijihifadhi yenyewe. Hii ni kwa maana kwamba, kuviingilia vitu visivyofahamika kiundani ni kujaribu kuvitibua asili yake na hivyo kusababisha madhara hasi kwa asili yenyewe na hata jamii inayoizunguka. Vitu hivi visivyofahamika vyema hata kwenye sayansi ya kisasa vipo vingi tu, na kiukweli baadhi ya dhana za kisayansi zimekuwa zinakanushwa mara kwa mara. Kwa mfano dhana kuu kuhusu “urithi wa geni” ijulikanayo kama “the central dogma” ambapo ilidhaniwa kuwa jeni moja hutengeneza protini moja, imekwisha kuthibitishwa kuwa siyo kweli (Waynne 2007).

Sayansi ya jadi inayachukulia mambo yote yasiyofahamika vyema katika mtazamo kuwa ulimwengu umeumbwa katika uwiano fulani na kwamba shughuri za binadamu zinatakiwa zisitibue uwiano huu wa asili. Hivyo basi jamii za kijadi zimekuwa na taasisi maalumu (kama vile wazee, waganga wa jadi au watabiri) zenye kutoa muongozo wa jinsi ya kushughurika na mambo yasiyofahamika vyema. Kwa sayansi ya kisasa mambo yote yasiyoelezeka na kufahamika vyema yanafaa kuchunguzwa hadi yafahamike vyema bila kujali madhara yake. Sayansi hii imejikita katika kufanya majaribio hata kama matokeo ya majaribio hayo hayafahamiki vyema. Kwa hali ilivyofikia sasa, tafiti za kisayansi hazifanyiki tu ili kutazama na kutaka kufahamu kinachotokea katika mambo mbalimbali bali kujaribu kubadili ufanyaji kazi wa mambo mbalimbali kama seli za uhai ili tu kuona jambo litakalotokea.

Chanzo kikuu cha elimu ya jadi ni mazingira yanoyozunguka jamii husika. Na ndio mimea inayopewa hadhi ya uhifadhi katika jamii ya watu wa Ruvuma inaweza kuwa tofauti na mimea inayopewa hadhi maalum na watu wa Pwani. Hii ni kwa sababu jamii hizi zinazungukwa na mazingira tofauti. Jambo la kutilia maanani ni kuwa, uhusishwaji wa elimu hii ya jadi na utamaduni pamoja na Imani za jamii fulani, isitumike kama kigezo cha kufifisha umuhimu wa elimu hii hasa katika mazingira ya sasa ya uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na shughuri mbalimbali za kibinadamu, magonjwa mengi, mabadiliko ya tabia nchi na hata upungufu wa chakula. 
 
elimu ya jadi humfunganisha mtu na mazingira yake.

Tunawezaje kuitumia elimu ya jadi katika zama hizi za sayansi na teknolojia?
Jinsi watu wa asili walivyojifunza elimu yao inatoa mwanga wa umuhimu wa elimu hii. Elimu hii haikupatikana kwa njia moja tu ya kushibisha akili, elimu hii iligusa sehemu kuu nne za maisha ya mtu. Iligusa akili, iligusa pia hisia, roho (imani) na pia nguvu za kimwili (utendaji). Kama tutaweza kuihusisha aina hii ya elimu katika mfumo wetu rasmi wa elimu ya kisasa, itaongeza sana ubora hasa katika kipengele cha ufanisi wa watu wanaohitimu mafunzo katika kukabili changamoto mbalimbali za maisha.

Kati ya tabia kuu za elimu ya jadi ni kusisitiza uwajibikaji wa kijumla. Hii ni kuhimiza ushirikiano wa jamii nzima katika kuheshimu ardhi na mazingira, kuheshimu pia uwiano na utegemeanaji wa viumbe na pia umuhimu wa kutumia tu kile kinachohitajika. Ingawa Tanzania ni moja kati ya nchi zinazoongoza katika kutenga ardhi kwa ajili ya uhifadhi (kwa takwimu za 2011 za shirika la maendeleo la umoja wa mataifa, kilometa za eneo takribani 250,000 za ardhi yote imetengwa kwa ajili ya uhifadhi ambayo ni takribani 27%, ikijumuisha mapori ya hifadhi, mbuga za wanyama n.k), lakini ni moja kati ya nchi zinazokabiliwa na upotevu mkubwa wa maliasili (aina za mimea takribani 240 ipo katika hatari ya kutoweka kati ya aina za mimea takribani 10,000 inayopatikana Tanzania, wanyama (mamalia) 42 kati ya 316, na ndege 33 kati ya 229).

Kasi hii ya upotevu wa maliasili inaweza kuhusishwa kwa kiasi fulani na kushindwa kwa elimu ya uhifadhi ya kimagharibi ambayo inatolewa kwa jamii ambazo tayari zilikuwa na mifumo yao thabiti ya uhifadhi iliyokuwa inatolewa na elimu yao ya jadi. Hebu tazama tu katika jamii tunayoishi sasa jinsi ambavyo chochote ambacho ni cha uma kinavyo chukuliwa. Wala tusishangae jinsi jamii hizi zinavyoshindwa kujali mazingira na kupelekea madhara kama tuliyonayo sasa. Hivyo kuingiza katika mitaala yetu jinsi nzuri ya uhifadhi shirikishi ni moja ya njia ya kuunganisha elimu jadi nah ii ya kisasa.

Matumizi ya elimu ya jadi katika elimu ya kisasa sio kitu kigeni duniani, na kwa hivyo sio kazi ngumu kufanyika. Tukichukulia mifano iliyowazi katika nyanja ya utengenezaji wa madawa, wanasayansi wa kimagharibi ambao hufanya kazi katika makampuni makubwa ya utafiti na utengenezaji wa dawa za maradhi mbalimbali, hufanyia kazi kwa ukaribu elimu ya jadi kutoka kwa wenyeji wa maeneo inakopatikana misitu mbalimbali hasa Afrika, Asia na Amerika Kusini. Watu wanaoishi katika maeneo inakopatikana misitu ya kitropiki wameweza kukusanya ujuzi na ufahamu mwingi kuhusu matumizi ya mimea mbalimbali kama dawa. Hivyo basi kwa kutambua hilo, makampuni ya dawa hukusanya taarifa hizi kutoka kwa wenyeji na kuzitumia katika tafiti zao za dawa mbalimbali. Huu ni ushahidi tosha kwamba, hata leo, elimu ya jadi inanafasi kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia yetu. Hili tunaweza kulitanua kutoka katika tafiti za madawa hadi katika nyanja nyingine za elimu tunayoitoa sasa. 

Wenyeji wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na majanga ya kiasili mara kwa mara kama vile vimbunga na matetemeko ya ardhi, huwa na ujuzi wa kusoma tabia za wanyama mbalimbali kama mbwa, ndege na hata nyoka katika kutabiri ujio wa majanga hayo ya asili. Kukosa ufahamu wa kujua namna ambavyo wanyama hawa hujua kutabiri majanga na namna ambavyo watu huweza kuwasoma kwa usahihi, visizuie kuiingiza elimu hii na nyingine kama hizi katika mifumo rasmi ya ufundishaji mashuleni. Tutumie ujuzi na ufahamu wa jamii za kijadi katika kuingiza mafundisho ya kinsi ya kufanya kilimo bora, ufugaji bora, elimu bora na hata utabibu. Tuache kujaribu kuzi “staarabisha” jamii zetu za kijadi.

Pamoja na yote ni lazima tukubali kwamba elimu ya kisasa inayo mazuri mengi lakini tusizipuuze changamoto zake. Kwa mfano migogoro mbalimbali kati ya wakaazi wa maeneo yanayozunguka hifadhi za kitaifa ambayo imeshapelekea madhara makubwa hata vifo, migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya kisiasa n.k inachangiwa sana na kujaribu kuleta majibu ya kisasa kwa changamoto za kijadi.

Yangu ni hayo, tujitafakari na pia tusisahau kamwe kwamba “asili ni mali”.

David Simiyu
0764843000



No comments:

Post a Comment