Friday 25 September 2015

VIUMBE VAMIZI (Invasive Species). The forgotten Evil.



Viumbe Vamizi (adui mkubwa wa ustawi wa viumbe asiye pewa kipaumbele).
Na Simiyu David
Mobile +255764843000 email: davidmsimiyu@gmail.com
Uharibifu wa makazi asili ya viumbe ni moja ya majanga makubwa ya kimazingira kuwahi kuikabili dunia. Kwa bahati mbaya madhara ya uharibifu wa makazi ya viumbe huwa ni ya muda mrefu na mara nyingi ni ya kudumu. Makazi ya asili yanapoharibiwa au kubadilishwa, viumbe wa eneo husika huwa katika hatari ya kutoweka. Mfano mzuri unapatikana katika nchi yetu, vyura wa Kihansi (Kihansi spray toads) ni vyura wasiopatikana sehemu nyingine yoyote duniani, na ni vyura wa ajabu sana, maana badala ya kutaga kama vyura wengine wao huzaa. Vyura hawa wako katika hatari ya kutoweka kwa kuwa makazi yao ya asili yalibadilishwa kutokana na mahitaji ya binadamu. Maporomoko asili yaliyokuwepo Kihansi yanatumika sasa kufua umeme na hivyo kufanya makazi ya vyura wa Kihansi yasifae tena kwa ustawi wa viumbe hawa adimu.
Shughuri za kibinadamu inatajwa kuwa ndiyo sababu kubwa kabisa ya uharibifu/ubadilishaji wa makazi asili ya viumbe. Shughuri za kilimo, uvuvi haramu, ufugaji wa mifugo mingi katika eneo moja, uchomaji misitu, ukuaji wa miji na shughuri nyingine nyingi za kibinadamu huharibu makazi ya viumbe. Mara nyingi sababu hii (shughuri za kibinadamu) ndiyo inayotiliwa mkazo sana na wanamazingira. Jitihada nyingi za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali zimeelekezwa katika kuelimisha jamii kuhusu madhara ya shughuri mbalimbali za binadamu kwa mazingira na jinsi ya kuweka uwiano kati ya maendeleo ya watu na ustawi wa mazingira.
Baraza la kimataifa la ustawi wa viumbe (Convention on Biological Diversity) ambalo Tanzania ni mwanachama wake, linataja sababu ya pili kubwa inayosababisha uharibifu wa makazi asili ya viumbe kuwa ni viumbe vamizi (invasive species). Janga hili la viumbe vamizi halija tiliwa sana mkazo hasa katika elimu ya jinsi ya kuzuia viumbe hivi.
Viumbe vamizi ni nini?
Viumbe hai wamegawanyika katika makundi  mbalimbali, kuna kundi la mimea, kundi la wanyama, kundi la fungi n.k. Viumbe hai wanaopatikana katika eneo fulani, wanaweza kuwa ni viumbe wa asili ya eneo hilo (native species) au wanaweza wasiwe wa asili yaani wageni katika eneo hilo (exotic/alien species). Viumbe vamizi ni viumbe wasio asili katika eneo wanaloishi na ambao huongezeka idadi na kustawi pasipo udhibiti na kubadili au kuharibu ustawi wa viumbe wengine katika eneo husika. Kwa maana hiyo, aina fulani ya kiumbe anaweza akawa sio wa asili katika eneo analoishi lakini pia asiwe kiumbe vamizi, lakini viumbe vamizi wote ni viumbe wasio asili katika maeneo wanayopatikana.
Katika Tanzania, kuna viumbe vamizi vingi. Kuwepo kwa wingi wa mimea na wanyama ambao ni vamizi katika Tanzania inashangaza kutokufahamika kwake kwa watu wengi. Kwa mujibu wa global invasive species database, Tanzania ina takribani viumbe vamizi 100. Baadhi ya viumbe ambao watu wengi tunawafahamu ni samaki aina ya sangara (Lates nilotica) katika ziwa victoria, Mimea aina ya magugu maji (Eichhornia crassipes), ndege aina ya kunguru (Indian house crow), mimea aina ya mishona nguo (Bidens pilosa) na viumbe wengine wengi (tembelea www.issg.org kupata viumbe wengine vamizi katika Tanzania).










Mashona nguo (Bidens Pilosa) ni moja kati ya mimea vamizi. Picha kwa hisani ya www.agrotico.net
 
Viumbe vamizi husambazwa zaidi na binadamu kutoka eneo moja hadi jingine. Binadamu husambaza viumbe hawa mara nyingi bila kufahamu kuwa anasafirisha viumbe. Kwa mfano mvuvi anaweza kuhamisha vifaa vyake vya uvuvi kutoka eneo moja kwenda jingine bila kujua kuwa vifaa hivyo vimebeba mayai ya samaki au mbegu za mimea. Mara nyingine binadamu hujikuta amesababisha uwepo wa viumbe vamizi baada ya kusafirisha kwa makusudi kiumbe fulani bila kujua kiumbe hicho kitakuja kuwa vamizi na kuathiri ustawi wa viumbe wengine. Kwa mfano, miaka ya 1950, enzi ya utawala wa kikoloni katika Afrika Mashariki, samaki aina ya Sangara (Lates nilotica) alipandikizwa katika ziwa Viktoria kutoka katika ziwa Albert huko Uganda kwa ajili ya kuongeza chakula kwa binadamu, matokeo yake Sangara amekua ni moja ya viumbe vamizi vilivyoleta madhara makubwa sana kwa mazingira ya ziwa hilo.
Kwanini viumbe vamizi hustawi zaidi ya viumbe wengine
Ustawi wa viumbe wasio wa-asili hadi kuwa viumbe vamizi pamoja na mambo mengine husababishwa sana na kutokuwapo na maadui wa kiumbe husika katika mazingira hayo ya ugenini. Kwa mfano kama swala walioko katika hifadhi ya Serengeti wangekuwa hawana maadui zake wa asili kama samba na chui, kuna uwezekano swala hawa wakaongezeka sana idadi hadi kuathiri mfumo asili wa kiikolojia. Hivyo ni dhahiri kuwa bila mfumo wa asili wa kudhibiti usambaaji na idadi ya viumbe wageni katika eneo fulani ni dhahiri viumbe hawa wasio wenyeji watakuwa viumbe vamizi. Kwa mimea vamizi, ustawi wake hutegemeana sana na kuwepo na uharibifu wa uoto wa asili na kuacha nafasi wazi ambayo mimea hiivamizi huweza kuziba nafasi hiyo wazi kwa haraka na hivyo kuzuia urudishiaji wa uoto wa asili.
Athari za viumbe vamizi
Ziko athari mbalimbali ambazo zinaweza kuletwa na viumbe vamizi. Athari hizo ni pamoja na, kusababisha maradhi mapya katika eneo husika. Viumbe vamizi pia, ni moja ya vyanzo vikubwa sana vya kutoweka viumbe (extinction of species). Katika ziwa Viktoria kwa mfano, samaki aina ya sangara amesababisha kutoweka kwa aina takribani mia tatu (300) katika ziwa hilo.







Samaki sangara (Lates nilotica) akiwa anachuuzwa sokoni huko Uganda. Sangara ni kiumbe vamizi katika ziwa Viktoria na amesababisha kutoweka kwa jamii nyingi za viumbe katika ziwa hilo. Picha kwa hisani ya www.news.ugo.co.ug
Madhara mengine ni uharibifu na ubadilishaji wa makazi asili ya viumbe wa eneo fulani. Mfano mzuri ni magugu maji (Eichhornia crassipes) ambayo asili yake ni katika bara la Amerika ya kusini. Magugu maji yanapotanda juu ya maji, huzuia upatikanaji mzuri wa mwanga pamoja na hewa kwa viumbe waishiyo ndani ya maji.








Magugu maji yakiwa yametanda juu ya maji. Picha na vipin chandran www.apms.org
 
Athari nyingine ya viumbe vamizi ni ile ya gharama. Kama ambavyo tulishuhudia katika suala la kupambana na magugu maji, kiasi cha fedha kilichotumika ni kikubwa sana na pia muda ambao ilichukua hadi kuyapunguza magugu maji ulikua ni mrefu sana. Kwa mfano ilibidi kuingizwa nchini viumbe (hyacinth weevils) ambao walisaidia katika kuyapunguza magugu hayo katika kile kinachojulikana kama Biological control.
Tufanyaje ili kuzuia viumbe vamizi?
Sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 67(2) na ile ya uvuvi ya mwaka 2001, zinaelekeza kuwa si ruhusa kusafirisha na kusambaza viumbe kutoka eneo moja hadi linguine bila kuwa na ruhusa maalumu. Ni dhahiri kuwa madhara ya viumbe vamizi ni makubwa sana kwa mazingira, ingawa zipo njia mbalimbali za kupambana na viumbe vamizi kama vile kutumia viumbe hai wengine kudhibiti usambaaji wake (Biological control) na pia kutumia kemikali za sumu, lakini njia bora zaidi ni kuzuia uingiaji wake. Kama kila mmoja wetu atachukua tahadhari na hivyo kutohamisha kiumbe yoyote (mnyama au mmea) bila kuwa na uhakika kuwa kiumbe yule anapatikana pia katika maeneo unayomuhamishia basi tatizo la kusambaza viumbe vamizi litakwisha. Cha muhimu pia ni kuhakikisha vifaa kama vya uvuvi vinapohamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine vinahakikishwa kwanza hakuna mimea au kiumbe yoyote (hasa mayai) ambayo yatahama na vifaa hivyo.
Hitimisho
Viumbe wote duniani tunaishi kwa kutegemeana. Kama makazi ya viumbe (hata kama wanaonekana kwetu kuwa hawana manufaa) yataharibika, viumbe hao watakua katika hatari ya kupotea. Kiumbe anapotoweka, hata wale viumbe wengine ambao waliishi kwa kutegemea kiumbe yule pia watadhurika. Mnyororo huu utazunguka hadi ufike kwetu sisi binadamu ambao mwenyezi Mungu ametupatia akili na maarifa ya kutawala mazingira yetu. Ni wajibu wetu kupaza sauti zetu, kuhakikisha mazingira asili yanahifadhiwa kwa gharama yoyote, tuhakikishe makazi asili ya viumbe yanalindwa na hivyo kujihakikishia ustawi wa viumbe vyote. 
By the way, ASILI NI MALI.

Friday 4 September 2015

UHANDISI JENI NI NINI? JE! TUIKUBALI TEKNOLOJIA HII?



Matumizi ya mazao yaliyohandisiwa jeni (genetically modified crops): Afrika ikubali au ikatae?
Na David Mojo Simiyu
Kilimo ndiyo sekta muhimu katika jamii nyingi za kiafrika na nchi zingine zinazoendelea. Sekta hii inachangia takribani asilimia 35 ya pato la bara zima la Afrika huku ikiajiri zaidi ya asilimia 70 ya waafrika. Kumekuwepo na jitihada nyingi za kukiendeleza kilimo katika Afrika, lakini jitihada hizi zimekuwa zikigubikwa na changamoto kadhaa kama vile, uongezekaji wa kasi wa idadi ya watu, mabadiliko ya hali ya hewa, matatizo ya kiutawala, machafuko ya kisiasa na uhaba wa uwekezaji.
Katika azimio la Maputo la mwaka 2003 pamoja na lile tamko la viongozi wa umoja wa Afrika la mwaka 2009, kumeazimiwa kuwa Afrika iongeze uzalishaji wa chakula. Lakini bado kuna mamilioni ya watu leo hii katika Afrika walio katika hatari ya kufa kwa njaa. Inakadiriwa kuwa kuna watu milioni mbili wanaougua utapiamlo katika Africa wengi wao wakiwa watoto na wamama wajawazito. Takwimu za UNICEF za mwaka 2015 zinaonesha kuwa watoto zaidi ya laki mbili na ishirini (220,000) wanaugua utapiamlo mkali Tanzania bara pekee. Kwa mujibu wa takwimu hizo za UNICEF asilimia arobaini na mbili (42%) ya watoto wote wa Tanzania wamedumaa. Madhara haya ya utapiamlo yanasababishwa na ukosefu wa chakula cha kutosha lakini pia kutokupata chakula chenye lishe bora.
Baadhi ya jitihada zinazofanyika ili kupambana na janga la lishe duni kwa jamii za nchi zinazoendelea ni pamoja na;
1.      Kuleta misaada ya chakula kutoka nchi zilizoendelea.
2.      Kutoa fedha na ufadhili mwingine kwenda kwa taasisi za afya za nchi masikini.
3.      Kutia mkazo katika matumizi ya mbegu zilizo handisiwa (Genetically modified seeds).
Jitihada mbili za kwanza kati ya zilizotajwa hapo juu zimekuwa zikifanywa kwa miongo kadhaa sasa lakini hakujakuwa na maendeleo makubwa sana. Mpaka sasa kwa mfano Tanzania imeshindwa kabisa kufikia lengo la kwanza la milenia, lililo lenga kuondoa njaa na umasikini uliokithiri kufikia mwaka 2015.Nchi nyingi zilizoendelea kwa sasa zinaona jitihada ya tatu hapo juu ya kutumia mimea iliyo handisiwa jeni (GMOs), kuwa ndiyo jawabu sahihi la matatizo ya njaa katika Afrika na nchi nyingine.
Mimea iliyo handisiwa gini (GMOs) ni mimea iliyotokana na teknolojia ya kihandisi biolojia ya kubadilisha mfumo asili wa jeni (genes) za mimea ili kuzipandikizia uwezo fulani utakaokuwa na manufaa zaidi kwa binadamu. Kwa mfano, mimea inaweza kupandikizwa uwezo wa kuhimili ukame, au uwezo wa kustawi kwenye ardhi yenye kiwango kikubwa cha chumvi, au hata uwezo wa kuhimili magonjwa, wadudu na madawa ya kuua magugu.
Kwa maana hiyo, jamii inayoishi katika maeneo yenye ukame yanaweza kupanda mazao ya chakula na yakastawi hivyo kuepuka njaa. Pia hata kukiwa na ongezeko kubwa la watu na uhaba wa ardhi kwa ajili ya kilimo, bado mimea inaweza kuwekewa uwezo wa kuzaa mavuno mengi na kwa muda mfupi hata kutoka katika ardhi finyu na ambayo isingeweza kustawisha mimea ya kawaida.
Je! Ni salama kutumia mimea iliyo handisiwa?
Kumekuwa na mjadala mkali katika dunia yote kuhusu matumizi ya mimea iliyo handisiwa. Kumekuwa na watetezi wa teknolojia hii na wale wanaoipinga.Watetezi wa matumizi ya teknologia ya kuhandisi mimea, wanasimama upande huo kutokana na hoja kadhaa. Baadhi ya hoja za watetezi wa mimea iliyo handisiwa ni;
Upungufu wa ardhi inayofaa kwa kilimo
Wakati dunia inahitajika kuzalisha mara mbili ya chakula kinachozalishwa sasa ili kuweza kutosheleza mahitaji itakapofika mwaka 2050, hatuna uwezo wa kuongeza eneo la dunia linalofaa kwa uzalishaji wa chakula. Hii ni kutokana ongezeko la watu na makazi, lakini pia inatokana na hamu ya dunia kuhifadhi baadhi ya maeneo katika uasili wake. Watetezi wa GMOs wanasema technolojia ya kuhandisi mimea inatupatia fursa ya kusafisha maeneo ambayo kwa sasa hayafai kwa kilimo. Kwa mfano miti iitwayo poplar (Populus spp.) huweza kupewa uwezo wa kuondoa ardhini madini yenye madhara kwa binadamu katika kile kinachoitwa “phytoremediation”. Mimea ya mazao pia inaweza kuhandisiwa na ikastawi katika ardhi zenye chumvi kama zile zilizoko karibu sana na pwani, hivyo kuongeza maeneo yanayotumika kuzalisha chakula.
Ongezeko la idadi ya watu
Umoja wa mataifa unakadiria kuwa, kufikia mwaka 2050 dunia itakuwa na watu bilioni 8.92 kutoka zaidi kidogo ya bilioni 7 hivi sasa. Asilimia ishirini ya watu hao watakua wanaishi katika bara la Afrika. Kutokana na ukweli kuwa hata katika idadi ya sasa bado kuna idadi kubwa ya watu wanaoathirika na njaa, ni dhahiri kuwa hali itaendelea kuwa mbaya zaidi katika miongo michache ijayo. Jitihada nyinginezo za kukabili njaa katika Afrika na mataifa yanayoendelea kama zilivyoainishwa hapo awali, hazijaweza kukabili tatizo. Mimea iliyohandisiwa jeni inaweza kutoa mazao mengi zaidi hivyo kuweza kulisha watu wengi zaidi tofauti na mimea isiyohandisiwa. Mimea iliyohandisiwa jeni pia inaweza kupewa uwezo wa kuwa na lishe bora zaidi hivyo kutatua tatizo la utapimlo. Kwa mfano, mchele unaweza kupewa uwezo wa kumpatia binadamu vitamin A, katika mchele wa kawaida vitamin hizi hazipo kabisa.
Mabadiliko ya tabia nchi
Mabadiliko ya tabia nchi ni dhana inayojulikana vyema na wakulima wengi hasa katika nchi zinazoendelea ambao hutegemea mvua kwa ajili ya kustawisha mazao yao. Mabadiliko ya misimu ya mvua, mvua kuchelewa na kutokunyesha kwa kiwango stahili ni baadhi ya mabadiliko yanayolalamikiwa sana katika jamiii za wakulima. Teknolojia ya kuhandisi mimea itawawezesha wakulima kuwa na mazao yanayohimili ukame na hata joto kali hivyo kumhakikishia mkulima chakula cha kutosha hata kusipokuwa na mvua za kutosha.
Kuokoa gharama
Watetezi wa teknolojia ya kuhandisi jeni za mimea wanasema matumizi ya mimea iliyohandisiwa ni nafuu zaidi kwa mkulima zaidi ya mimea isiyohandisiwa. Hii ni kwa sababu wakulima hawatakuwa na gharama tena ya kununua madawa ya kuua wadudu waharibifu kwa kuwa mimea inaweza kupewa uwezo wa kujilinda yenyewe dhidi ya wadudu. Mimea pia huweza kupandikizwa uwezo wa kutodhurika na madawa ya kuuwa magugu na hivyo wakulima badala ya kutumia gharama kupalilia magugu, ataweza kumwagia shamba lote dawa itakayoua magugu yote na kuacha mazao yake. Kwa mfano kampuni ya Monsanto imeweza kutengeneza maharage ambayo yanauwezo wa kuhimili na kutodhurika na dawa ya kuua magugu inayotengenezwa na kampuni hiyo yenye jina la ‘Roundup’.
Changamoto hazikosekani kwenye teknolojia yoyote
Teknolojia yoyote ile ina madhara na faida, malengo makubwa wa wajuzi wa technolojia ni kupunguza madhara yake na kuongeza faida. Mwaka 2012 kwa mfano, kituo cha kisayansi kinachojulikana kama ‘the centre for science in public interest’ kiliainisha mifano mingi ya magugu na wadudu ambao walijijengea usugu dhidi ya madawa yanayotumika kuwaua. Madawa haya tunayotumia mashambani huua pia wadudu wengi ambao sio waharibifu kwa mazao na ambao wanafaida katika mfumo wa ikolojia wa eneo husika. Hivyo kusema teknolojia ya kuhandisi jeni isitumike kwa kuwa ina madhara, si sawa kwa kuwa teknolojia hii ina faida zake, tena kubwa sana.
Teknolojia hii ni maboresho tu ya upandikizaji (breeding) ambao wakulima hufanya kila mara.
Wakulima kote duniani hupenda kupata mazao ambayo yana sifa anazozitaka. Kwa mfano mkulima angependa apate mavuno mengi, kama ni mahindi basi apate punje kubwa na nyeupe, kama ni mpunga basi utoe mchele mrefu, mnene na unaonukia. Kupata sifa hizi, mkulima anaweza kufanya upandizikizaji yaani akahakikisha uchavushaji unafanyika kati ya mimea yenye sifa anazozitaka halafu akaendelea kuchagua mbegu bora tu kwa ajili ya kupanda. Zoezi hili huchukua miaka, lakini teknolojia ya uhandisi jeni za mimea hufanikisha zoezi hili kwa muda mfupi tu. Zile jeni za mmea wenye sifa inayotakiwa zinachukuliwa na kuhamishiwa kwenye mmea mwingine wenye sifa nyingine inayotakiwa pia, hivyo kupata mchanganyiko wa sifa nyingi stahili kwenye mmea mmoja. Mmea huu huachwa uzae mbegu na mbegu hizi zitakua na jeni mchanganyiko zenye kumpatia mkulima sifa zote anazohitaji.
 Wapinzani wa teknolojia ya uhandisi jeni wa mimea wana maoni tofauti.
Pamoja na faida nyingi na utetezi unaoainishwa na watetezi wa GMOs katika nchi zinazoendielea, kuna sauti nyingi zinazopazwa kuhusu madhara ya kuruhusu matumizi ya mimea iliyohandisiwa. Ijulikane pia kuwa, upinzani wa matumizi ya GMOs upo pia katika nchi zilizoendelea. Watu wengi tu kutoka Marekani na Ulaya wanapinga matumizi ya GMOs.
Baadhi ya madhara yanatoainishwa na wapinzani wa matumizi ya mimea iliyohandisiwa ni;
Madhara kwa viumbe wasiokusudiwa
Mwaka 1999 katika Makala iliyochapishwa na jarida la kisayansi linaloheshimika sana duniani la Nature ilitoa matokeo ya utafiti uliofanyika na kuonesha mahindi yaliyohandisiwa na kupandikizwa jeni za bacteria aitwae Bacillus thuringiensis ili kupata uwezo wa kuua wadudu waharibifu, yalisababisha vifo kwa vipepeo ambao chakula chake wala sio mahindi. Hii inaashiria kuwa vipepeo hawa walikufa kutokana na poleni iliyopeperushwa kutoka kwenye mahindi haya yaliyohandisiwa. Swali ni je, madhara haya yaliyowapata vipepeo hayawezi kutupata binanadamu na viumbe wengine? Huenda matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni ikaleta madhara makubwa kwa mazingira zaidi ya faida tunayoitafuta.
Matajiri kuhodhi sekta ya kilimo
Utafiti, utengenezaji na usambaji wa mimea iliyohandisiwa jeni ni mchakato ambao unagharama kubwa mno. Wakulima na hata makampuni katika nchi zinazoendelea hawana uwezo wa kutengeneza mbegu zao wenyewe hivyo biashara hii hufanywa na makampuni yenye utajiri mkubwa kutoka katika nchi za dunia ya kwanza. Teknolojia inayohusika pamoja na mimea yenyewe iliyohandisiwa jeni vimekatiwa hati miliki. Hii ina maana kuwa hata nchi zetu zingetaka kutengeneza mimea hii, hazitaruhusiwa na makampuni yenye hati miliki ya teknolojia hii. Kwa ufupi ni kuwa kilimo kitakachotegemea GMO kitaendeshwa na kumilikiwa na makampuni ya nje. Makampuni haya yataamua bei ya mbegu na aina za mbegu zinazotakiwa na wakulima wa Tanzania. Siku tukiwakorofisha watagoma kutuuzia mbegu na kwa kuwa ardhi yetu itakuwa imeshakuwa tegemezi kwa GMO, itatubidi tuwapigie magoti na tujishushe hadhi yetu. Mataifa ya Afrika yana kila sababu ya kukataa msukumo wa kukubali matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni.


Kuharibu muingiliano wa jeni kati ya mimea
Madhara mengine ya matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni inatokana na muingiliano ambao upo kiasili kati ya mimea mingi ya mazao na mimea ya mwitu yenye ‘undugu’ nayo (wild relatives of crops). Katika maeneo mengi kunakuwapo na mimea ambayo inauhusiano wa karibu na mimea ya mazao. Kwa mfano Tanzania kunamimea yenye uhusiano wa karibu na kahawa. Ukaribu wa mimea ya aina hii na mazao huwezesha muingiliano wa kijeni kati yao. Jeni kutoka kwenye mimea ya mwitu huweza kuingia kwenye jeni za zao lenye uhusiano wa karibu na mmea mwitu husika. Hivyo basi jeni yenye kuleta uhimili wa dawa za kuua magugu kwa mfano, inaweza kuhamia kwenye mimea mwitu kutoka kwenye mazao yaliyohandisiwa. Jeni hii ikishaingia kwenye mimea ya mwitu ni ngumu sana kuidhibiti isisambae. Jeni kutoka kwenye mazao yaliyohandisiwa zinaweza pia kudhoofisha ustawi wa mimea ya mwitu na hivyo kuathiri bioanuai. Jaribu kujiuliza itakuaje jeni mbalimbali zilizopandikizwa katika mimea zitahamia kwa mimea mwitu mbalimbali.
Watengenezaji wa GMOs wanadai kuwa muingiliano wa jeni katika mimea umekuwa ukifanyika katika hali ya kawaida siku zote. Lakini je, imewahi kutokea katika hali ya kawaida bakteria akaingiliana na mmea (hybridization)? Kwa kuwa teknolojia hii inaweza kuhamisha jeni kutoka viumbe mbalimbali kama vile bakteria, wadudu na hata wanyama kwenda kwa mimea, ni dhahiri baada ya muda tutakua na mkanganyiko mkubwa katika vyakula tunavyokula.
Madhara ya kiafya
Mwaka 2012 mwanasayansi Gilles-Eric Seralini na wenzake, walichapisha matokeo ya utafiti wao uliochukua miaka miwili katika jarida maarufu liitwalo ‘The Journal of Food and Chemical Toxicology’ uliioonesha madhara makubwa ya matumizi ya vyakula vinavyotokana na mimea iliyohandisiwa jeni pamoja na sumu ya glyphosate (ambayo ipo katika dawa ya kuulia magugu shambani ya roundup). Matokeo ya utafiti huo ulioitwa “madhara ya muda mrefu ya roundup na matumizi ya mahindi yaliyohandisiwa jeni kuhimili roundup”, yalionesha pasi na shaka kuwa, GMO zina madhara kwa maini na figo pamoja na kusababisha kansa. Kwa bahati mbaya sana, makampuni ya uhandisi wa kibaiolojia yaliupiga vita utafiti huu kwa kusaidiwa na serikali za ulaya na hivyo mwaka 2013 ikabidi jarida hili maarufu liuondoe utafiti huu kwenye chapisho lake.
Ilipofika mwaka Juni 2014, utafiti wa profesa Seralini na wenzake yalichapishwa tena katika jarida la sayansi ya mazingira la ulaya (Journal of Environmental Sciences Europe, Volume 26:14). Na kwa utafiti huo uliofanyika kwa panya imeonesha na kuthibitisha kisayansi uhusiano mkubwa uliopo kati ya mahindi yaliyohandisiwa jeni pamoja na dawa ya kuulia magugu ya Roundup, dhidi ya afya ya mifumo ya mamalia. Watafiti hawa wameonesha pia kuwa, masalia ya sumu ya glyphosate katika mimea inayoliwa yanauwezo wa kusababisha madhara ya kiafya kwa walaji. (utafiti huu unapatikana katika wavuti wa http://www.enveurope.com/content/pdf/s12302-014-0014-5.pdf au http://www.enveurope.com/content/26/1/14).
Pamoja na kuwa asilimia kubwa ya mimea iliyohandisiwa jeni katika nchi ya Marekani (ambapo kwa mwaka 2012, 93% ya soya na 88% ya mahindi yalikua yamehandisiwa jeni) hutumika zaidi kulisha wanyama, lakini sumu yoyote iliyoliwa na wanyama hubaki mwilini mwao na kuathiri maradufu wale watakaokula wanyama hawa. Kanuni hii huitwa biomagnification. Kwa bahati mbaya mazao yaliyohandisiwa kuhimili dawa za magugu yanapewa uwezo wa kupokea sumu hiyo bila kudhurika. Hii ina maana kuwa sumu hiyo huendelea kubaki mwilini mwa mmea, ha hivyo myama yeyote atakayekula mmea huo hula pia na sumu hiyo, na binadamu anapokula mnyama aliyekula mmea huo nae hupata athari. Kiwango cha athari hii huendelea kuongezeka kwa kadri mnyororo huu wa lishe unavyoongezeka (biomagnification).
Moja ya sumu ambayo hutumika katika madawa ya kuua magugu ni ‘glyphosate’. Utafiti unaonesha sumu hii ina madhara mengi katika afya ya binadamu. Glyphosate huingilia mfumo wa ‘hormones’ katika mwili (endocrine disruptor) na hivyo kusababisha matatizo kama kisukari, ugonjwa wa figo, kupanda kwa pressure ya damu, kuongezeka sana uzito, ugumba, kupungukiwa nguvu za kiume, kansa (ya matiti, tezi dume, ini, ubongo), ukuaji nk. Dr Nancy Swanson wa Marekani ameweza kuonesha pia kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni na magonjwa ya viungo mbalimbali vya mwili (soma matokeo ya utafiti wa Dr. Swanson katika wavuti wa http://people.csail.mit.edu/seneff/Swanson_et_al_2014.pdf).
Ushahidi zaidi wa madhara ya kiafya hasa wa sumu ya glyphosate ambayo inatumika katika dawa ya kuuwa magugu ya Roundup na ambayo huwepo katika mimea iliyohandisiwa jeni ili kutodhurika na dawa hiyo, umetolewa katika tafiti mbalimbali duniani. Utafiti wa Samsel na Seneff mwaka 2013, unaonesha wazi jinsi sumu hii inavyoathiri mifumo ya mwili kwa kuingilia njia za kifiziolojia za vichocheo viitwavyo kwa ujumla Cytochrome P450 (CYP) pathways. Uharibifu wa vichocheo hivi vinavyohusika pamoja na kazi nyingine asilimia 75 ya ‘organic molecules oxidation’, usafirishaji wa madini ya salfa (sulphate transport) katika majimaji ya damu (serum) na pia utengenezaji wa ‘aromatic amino acid’ katika bacteria wanaoishi katika utumbo mpana. Kuingilia shughuri hizi za mwili husababisha madhara ya kiafya baada ya muda mrefu kama vile magonjwa ya mfumo wa chakula, magonjwa ya moyo, unene, saratani, autism, Alzheimer’s pamoja na ugumba (soma zaidi utafiti huu katika wavuti wa http://responsibletechnology.org/media/Glyphosate_II_Samsel-Seneff%281%29.pdf). Utafiti wa Kruger 2013, umeonesha pia glyphosate huua bakteria wenye manufaa katika miili ya farasi na ng’ombe wakati Shehata na wenzake 2012, waligundua sumu hii huua bakteria wenye manufaa katika kuku. Kutokuwepo kwa bakteria hawa katika miili ya wanyama husababisha magonjwa kadhaa katika mfumo wa chakula mfano ‘stomach inflammation.
Tafiti zinazoonesha madhara ya glyphosate katika miili ya wanyama (mamalia na ndege) zipo nyingi na zinapatikana kirahisi katika wavuti mbalimbali. Ombi langu ni kuwa, ingawa pia kuna tafiti zinazoonesha kutokuwapo na madhara ya moja kwa moja ya mimea iliyohandisiwa jeni kwa afya ya binadamu, lakini kupuuza tafiti za kisayansi zinazoonesha madhara ya mimea hii itakuwa ni kosa. Tunapaswa kama nchi, na hasa sisi wananchi ambao ndio tutakuwa wahanga wa madhara ya mimea hii, kuwa na taarifa sahihi juu ya matumizi ya mimea hii. Hofu yangu kubwa ni kutogeuzwa majaribio.
JE TANZANIA TUTUMIE GMOs?
Ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo haya tuyaonayo ya binadamu na ustaarabu wake uliletwa na maendeleo ya kilimo. Lakini maendeleo yoyote lazima yaongozwe katika muelekeo sahihi hasa katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.
Madhara yanayotajwa na wapinzani wa mimea iliyohandisiwa jeni yanagusa moja kwa moja uhai wetu kama binadamu na ustawi wa mazingira yetu. Wale wanaotetea matumizi ya mimea hii mara zote wamekuwa wakipinga kwa jitihada kubwa mawazo ya wanaopinga GMO. Kwa mfano wanasema kuwa hakuna madhara ya kiafya kwa binadamu yaliyolipotiwa kuwa yanatokana na matumizi ya moja kwa moja ya GMOs. Lakini tunaposhughurika na jambo linalohusu uhai na ustawi wa binadamu, hatuhitaji ushahidi kuwa kitu hiki kinamadhara, bali kitu kitaruhusiwa kama kuna ushahidi kuwa hakina madhara. Na hii sio kazi ya walaji kuthibitisha kuwa GMO zina madhara, nadhani ni kazi ya makampuni haya makubwa kufanya tafiti na wathibitishe kuwa GMO hazina madhara.
Tuzungumzie pia suala nyeti la tatizo la njaa na utapiamlo. Tatizo hili ndilo limekuwa likitumiwa sana na nchi za magharibi pamoja na makampuni makubwa duniani ya uhandisi biolojia kuzitaka nchi zinazoendelea kuanza kutumia mimea iliyohandisiwa jeni. Lakini takwimu za uzalishaji chakula duniani zinaonesha kuwa dunia haina tatizo la uzalishaji wa chakula. Chakula kinachozalishwa kwa sasa duniani ni zaidi mara moja na nusu (1 ½) ya kiasi kinachotakiwa kuwalisha watu wote duniani. Hiki ni chakula kinachotosha kulisha watu bilioni kumi (idadi ya watu inayotazamiwa kuwepo mwaka 2050). Kwa maana hiyo, ni kuwa tatizo la njaa katika nchi zinazoendelea linatokana na umasikini pamoja na mfumo mbovu wa usambazaji wa chakula. Tatizo sio uwepo wa chakula, ila ni vipi kinawafikia ambao hawana.
Hitimisho
Kwa mtazamo rahisi ni kuwa, shinikizo kubwa tunalopewa ili kukubali matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni linasukumwa zaidi na sababu za kibiashara. Ingawa baadhi ya nchi za kiafrika zimeshakubali matumizi ya mimea hii, kwa Tanzania na watu wake teknolojia hii inapaswa kupewa muda zaidi ili tafiti nyingi zaidi zifanyike na hivyo kuthibitisha usalama wa mimea hii au jinsi ya kupunguza madhara yake. Hii ni kutokana na hali halisi kuwa, nchi hii ni kati ya nchi chache katika ukanda wa SADC zinazojitosheleza kwa chakula, kinachotakiwa ni kuelimisha zaidi wananchi ili wapende kula milo yenye lishe za protein, madini na vitamin pia kama vile mboga za majani, dagaa, maziwa, maharage (hasa ya soya) na chumvi iliyotiwa madini ya ‘iodine’. Hii itasaidia kupambana ukali wa janga la utapiamlo.
Mwaka 1998, wanasayansi 24 kutoka Afrika waliohudhuria mkutano wa umoja wa mataifa waliandika waraka mahususi uliosema “tunapinga vikali matumizi ya picha zinazoonesha watoto masikini na wenye njaa wa kiafrika zinazotumika na makampuni makubwa kusukuma matumizi ya teknolojia ambayo siyo salama, si rafiki kwa mazingira na isiyokuwa na faida za kiuchumi kwetu. Hatuamini kama teknolojia ya uhandisi jeni kama itasaidia wakulima wetu kuzalisha chakula kinachohitajika katika karne ya 21. Badala yake tunafikiri teknolojia hii itaharibu mazingira, elimu yetu ya asili na mfumo endelevu wa kilimo ambao wakulima wetu wameuendeleza kwa milenia kadhaa na kwamba teknolojia hii itadumaza uwezo wetu wa kujitengenezea chakula”
Kama malengo ya makubaliano ya Cartagena (Cartagena Protocol on Biosafety) ya mwaka 2003, ni jukumu la kila nchi hasa zinazoendelea kutengeneza sera madhubuti zitakazolinda mifumo yetu ya asili ya ukulima dhidi ya matumizi ambayo usalama wake unatiliwa shaka. Hivi inawezekanaje watu wanje ya Afrika walio maelfu ya kilometa kutoka kwenye mashamba yetu wakajua zaidi kuhusu kilimo chetu kuliko sisi? Au ndo tukumbuke ule usemi wa Dwight D. Eisenhower aliyesema “ukulima ni mwepesi sana kama jembe lako ni kalamu na umekaa maili nyingi kutoka shambani”
Mwandishi wa Makala hii ni mwajiriwa wa idara ya biolojia katika chuo kikuu cha kikatoliki Mwenge, Moshi-Tanzania. Kwa sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika sayansi ya mimea katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Ni mkereketwa wa mazingira asili.