Matumizi ya mazao yaliyohandisiwa jeni (genetically modified crops): Afrika
ikubali au ikatae?
Na David Mojo Simiyu
Kilimo ndiyo sekta muhimu katika
jamii nyingi za kiafrika na nchi zingine zinazoendelea. Sekta hii inachangia
takribani asilimia 35 ya pato la bara zima la Afrika huku ikiajiri zaidi ya
asilimia 70 ya waafrika. Kumekuwepo na jitihada nyingi za kukiendeleza kilimo
katika Afrika, lakini jitihada hizi zimekuwa zikigubikwa na changamoto kadhaa
kama vile, uongezekaji wa kasi wa idadi ya watu, mabadiliko ya hali ya hewa,
matatizo ya kiutawala, machafuko ya kisiasa na uhaba wa uwekezaji.
Katika azimio la Maputo la mwaka 2003
pamoja na lile tamko la viongozi wa umoja wa Afrika la mwaka 2009, kumeazimiwa
kuwa Afrika iongeze uzalishaji wa chakula. Lakini bado kuna mamilioni ya watu
leo hii katika Afrika walio katika hatari ya kufa kwa njaa. Inakadiriwa kuwa
kuna watu milioni mbili wanaougua utapiamlo katika Africa wengi wao wakiwa
watoto na wamama wajawazito. Takwimu za UNICEF za mwaka 2015 zinaonesha kuwa
watoto zaidi ya laki mbili na ishirini (220,000) wanaugua utapiamlo mkali
Tanzania bara pekee. Kwa mujibu wa takwimu hizo za UNICEF asilimia arobaini na
mbili (42%) ya watoto wote wa Tanzania wamedumaa. Madhara haya ya utapiamlo
yanasababishwa na ukosefu wa chakula cha kutosha lakini pia kutokupata chakula
chenye lishe bora.
Baadhi ya jitihada zinazofanyika ili
kupambana na janga la lishe duni kwa jamii za nchi zinazoendelea ni pamoja na;
1. Kuleta misaada ya chakula kutoka nchi
zilizoendelea.
2. Kutoa fedha na ufadhili mwingine
kwenda kwa taasisi za afya za nchi masikini.
3. Kutia mkazo katika matumizi ya mbegu
zilizo handisiwa (Genetically modified seeds).
Jitihada mbili za kwanza kati ya
zilizotajwa hapo juu zimekuwa zikifanywa kwa miongo kadhaa sasa lakini
hakujakuwa na maendeleo makubwa sana. Mpaka sasa kwa mfano Tanzania imeshindwa
kabisa kufikia lengo la kwanza la milenia, lililo lenga kuondoa njaa na
umasikini uliokithiri kufikia mwaka 2015.Nchi nyingi zilizoendelea kwa sasa
zinaona jitihada ya tatu hapo juu ya kutumia mimea iliyo handisiwa jeni (GMOs),
kuwa ndiyo jawabu sahihi la matatizo ya njaa katika Afrika na nchi nyingine.
Mimea iliyo handisiwa gini (GMOs) ni
mimea iliyotokana na teknolojia ya kihandisi biolojia ya kubadilisha mfumo
asili wa jeni (genes) za mimea ili kuzipandikizia uwezo fulani utakaokuwa na
manufaa zaidi kwa binadamu. Kwa mfano, mimea inaweza kupandikizwa uwezo wa
kuhimili ukame, au uwezo wa kustawi kwenye ardhi yenye kiwango kikubwa cha
chumvi, au hata uwezo wa kuhimili magonjwa, wadudu na madawa ya kuua magugu.
Kwa maana hiyo, jamii inayoishi
katika maeneo yenye ukame yanaweza kupanda mazao ya chakula na yakastawi hivyo
kuepuka njaa. Pia hata kukiwa na ongezeko kubwa la watu na uhaba wa ardhi kwa
ajili ya kilimo, bado mimea inaweza kuwekewa uwezo wa kuzaa mavuno mengi na kwa
muda mfupi hata kutoka katika ardhi finyu na ambayo isingeweza kustawisha mimea
ya kawaida.
Je! Ni salama kutumia mimea iliyo handisiwa?
Kumekuwa na mjadala mkali katika
dunia yote kuhusu matumizi ya mimea iliyo handisiwa. Kumekuwa na watetezi wa
teknolojia hii na wale wanaoipinga.Watetezi wa matumizi ya teknologia ya
kuhandisi mimea, wanasimama upande huo kutokana na hoja kadhaa. Baadhi ya hoja
za watetezi wa mimea iliyo handisiwa ni;
Upungufu wa ardhi inayofaa kwa kilimo
Wakati dunia inahitajika kuzalisha
mara mbili ya chakula kinachozalishwa sasa ili kuweza kutosheleza mahitaji
itakapofika mwaka 2050, hatuna uwezo wa kuongeza eneo la dunia linalofaa kwa
uzalishaji wa chakula. Hii ni kutokana ongezeko la watu na makazi, lakini pia
inatokana na hamu ya dunia kuhifadhi baadhi ya maeneo katika uasili wake.
Watetezi wa GMOs wanasema technolojia ya kuhandisi mimea inatupatia fursa ya
kusafisha maeneo ambayo kwa sasa hayafai kwa kilimo. Kwa mfano miti iitwayo
poplar (Populus spp.) huweza kupewa uwezo wa kuondoa ardhini
madini yenye madhara kwa binadamu katika kile kinachoitwa “phytoremediation”.
Mimea ya mazao pia inaweza kuhandisiwa na ikastawi katika ardhi zenye chumvi
kama zile zilizoko karibu sana na pwani, hivyo kuongeza maeneo yanayotumika
kuzalisha chakula.
Ongezeko la idadi ya watu
Umoja wa mataifa unakadiria kuwa,
kufikia mwaka 2050 dunia itakuwa na watu bilioni 8.92 kutoka zaidi kidogo ya
bilioni 7 hivi sasa. Asilimia ishirini ya watu hao watakua wanaishi katika bara
la Afrika. Kutokana na ukweli kuwa hata katika idadi ya sasa bado kuna idadi
kubwa ya watu wanaoathirika na njaa, ni dhahiri kuwa hali itaendelea kuwa mbaya
zaidi katika miongo michache ijayo. Jitihada nyinginezo za kukabili njaa katika
Afrika na mataifa yanayoendelea kama zilivyoainishwa hapo awali, hazijaweza
kukabili tatizo. Mimea iliyohandisiwa jeni inaweza kutoa mazao mengi zaidi
hivyo kuweza kulisha watu wengi zaidi tofauti na mimea isiyohandisiwa. Mimea
iliyohandisiwa jeni pia inaweza kupewa uwezo wa kuwa na lishe bora zaidi hivyo
kutatua tatizo la utapimlo. Kwa mfano, mchele unaweza kupewa uwezo wa kumpatia
binadamu vitamin A, katika mchele wa kawaida vitamin hizi hazipo kabisa.
Mabadiliko ya tabia nchi
Mabadiliko ya tabia nchi ni dhana
inayojulikana vyema na wakulima wengi hasa katika nchi zinazoendelea ambao
hutegemea mvua kwa ajili ya kustawisha mazao yao. Mabadiliko ya misimu ya mvua,
mvua kuchelewa na kutokunyesha kwa kiwango stahili ni baadhi ya mabadiliko
yanayolalamikiwa sana katika jamiii za wakulima. Teknolojia ya kuhandisi mimea
itawawezesha wakulima kuwa na mazao yanayohimili ukame na hata joto kali hivyo
kumhakikishia mkulima chakula cha kutosha hata kusipokuwa na mvua za kutosha.
Kuokoa gharama
Watetezi wa teknolojia ya kuhandisi jeni
za mimea wanasema matumizi ya mimea iliyohandisiwa ni nafuu zaidi kwa mkulima
zaidi ya mimea isiyohandisiwa. Hii ni kwa sababu wakulima hawatakuwa na gharama
tena ya kununua madawa ya kuua wadudu waharibifu kwa kuwa mimea inaweza kupewa
uwezo wa kujilinda yenyewe dhidi ya wadudu. Mimea pia huweza kupandikizwa uwezo
wa kutodhurika na madawa ya kuuwa magugu na hivyo wakulima badala ya kutumia
gharama kupalilia magugu, ataweza kumwagia shamba lote dawa itakayoua magugu
yote na kuacha mazao yake. Kwa mfano kampuni ya Monsanto imeweza kutengeneza
maharage ambayo yanauwezo wa kuhimili na kutodhurika na dawa ya kuua magugu
inayotengenezwa na kampuni hiyo yenye jina la ‘Roundup’.
Changamoto hazikosekani kwenye teknolojia yoyote
Teknolojia yoyote ile ina madhara na
faida, malengo makubwa wa wajuzi wa technolojia ni kupunguza madhara yake na
kuongeza faida. Mwaka 2012 kwa mfano, kituo cha kisayansi kinachojulikana kama
‘the centre for science in public interest’ kiliainisha mifano mingi ya magugu
na wadudu ambao walijijengea usugu dhidi ya madawa yanayotumika kuwaua. Madawa
haya tunayotumia mashambani huua pia wadudu wengi ambao sio waharibifu kwa
mazao na ambao wanafaida katika mfumo wa ikolojia wa eneo husika. Hivyo kusema
teknolojia ya kuhandisi jeni isitumike kwa kuwa ina madhara, si sawa kwa kuwa
teknolojia hii ina faida zake, tena kubwa sana.
Teknolojia hii ni maboresho tu ya upandikizaji (breeding) ambao wakulima
hufanya kila mara.
Wakulima kote duniani hupenda kupata
mazao ambayo yana sifa anazozitaka. Kwa mfano mkulima angependa apate mavuno
mengi, kama ni mahindi basi apate punje kubwa na nyeupe, kama ni mpunga basi
utoe mchele mrefu, mnene na unaonukia. Kupata sifa hizi, mkulima anaweza
kufanya upandizikizaji yaani akahakikisha uchavushaji unafanyika kati ya mimea
yenye sifa anazozitaka halafu akaendelea kuchagua mbegu bora tu kwa ajili ya kupanda.
Zoezi hili huchukua miaka, lakini teknolojia ya uhandisi jeni za mimea
hufanikisha zoezi hili kwa muda mfupi tu. Zile jeni za mmea wenye sifa
inayotakiwa zinachukuliwa na kuhamishiwa kwenye mmea mwingine wenye sifa
nyingine inayotakiwa pia, hivyo kupata mchanganyiko wa sifa nyingi stahili
kwenye mmea mmoja. Mmea huu huachwa uzae mbegu na mbegu hizi zitakua na jeni
mchanganyiko zenye kumpatia mkulima sifa zote anazohitaji.
Wapinzani wa teknolojia ya
uhandisi jeni wa mimea wana maoni tofauti.
Pamoja na faida nyingi na utetezi
unaoainishwa na watetezi wa GMOs katika nchi zinazoendielea, kuna sauti nyingi
zinazopazwa kuhusu madhara ya kuruhusu matumizi ya mimea iliyohandisiwa.
Ijulikane pia kuwa, upinzani wa matumizi ya GMOs upo pia katika nchi zilizoendelea.
Watu wengi tu kutoka Marekani na Ulaya wanapinga matumizi ya GMOs.
Baadhi ya madhara yanatoainishwa na
wapinzani wa matumizi ya mimea iliyohandisiwa ni;
Madhara kwa viumbe wasiokusudiwa
Mwaka 1999 katika Makala
iliyochapishwa na jarida la kisayansi linaloheshimika sana duniani la Nature ilitoa matokeo ya utafiti
uliofanyika na kuonesha mahindi yaliyohandisiwa na kupandikizwa jeni za
bacteria aitwae Bacillus thuringiensis ili
kupata uwezo wa kuua wadudu waharibifu, yalisababisha vifo kwa vipepeo ambao chakula chake wala sio mahindi. Hii
inaashiria kuwa vipepeo hawa walikufa kutokana na poleni iliyopeperushwa kutoka
kwenye mahindi haya yaliyohandisiwa. Swali ni je, madhara haya yaliyowapata
vipepeo hayawezi kutupata binanadamu na viumbe wengine? Huenda matumizi ya
mimea iliyohandisiwa jeni ikaleta madhara makubwa kwa mazingira zaidi ya faida
tunayoitafuta.
Matajiri kuhodhi sekta ya kilimo
Utafiti, utengenezaji na usambaji wa
mimea iliyohandisiwa jeni ni mchakato ambao unagharama kubwa mno. Wakulima na
hata makampuni katika nchi zinazoendelea hawana uwezo wa kutengeneza mbegu zao
wenyewe hivyo biashara hii hufanywa na makampuni yenye utajiri mkubwa kutoka
katika nchi za dunia ya kwanza. Teknolojia inayohusika pamoja na mimea yenyewe
iliyohandisiwa jeni vimekatiwa hati miliki. Hii ina maana kuwa hata nchi zetu
zingetaka kutengeneza mimea hii, hazitaruhusiwa na makampuni yenye hati miliki
ya teknolojia hii. Kwa ufupi ni kuwa kilimo kitakachotegemea GMO kitaendeshwa
na kumilikiwa na makampuni ya nje. Makampuni haya yataamua bei ya mbegu na aina
za mbegu zinazotakiwa na wakulima wa Tanzania. Siku tukiwakorofisha watagoma
kutuuzia mbegu na kwa kuwa ardhi yetu itakuwa imeshakuwa tegemezi kwa GMO,
itatubidi tuwapigie magoti na tujishushe hadhi yetu. Mataifa ya Afrika yana
kila sababu ya kukataa msukumo wa kukubali matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni.
Kuharibu muingiliano wa jeni kati ya mimea
Madhara mengine ya matumizi ya mimea
iliyohandisiwa jeni inatokana na muingiliano ambao upo kiasili kati ya mimea
mingi ya mazao na mimea ya mwitu yenye ‘undugu’ nayo (wild relatives of crops).
Katika maeneo mengi kunakuwapo na mimea ambayo inauhusiano wa karibu na mimea
ya mazao. Kwa mfano Tanzania kunamimea yenye uhusiano wa karibu na kahawa.
Ukaribu wa mimea ya aina hii na mazao huwezesha muingiliano wa kijeni kati yao.
Jeni kutoka kwenye mimea ya mwitu huweza kuingia kwenye jeni za zao lenye uhusiano
wa karibu na mmea mwitu husika. Hivyo basi jeni yenye kuleta uhimili wa dawa za
kuua magugu kwa mfano, inaweza kuhamia kwenye mimea mwitu kutoka kwenye mazao
yaliyohandisiwa. Jeni hii ikishaingia kwenye mimea ya mwitu ni ngumu sana
kuidhibiti isisambae. Jeni kutoka kwenye mazao yaliyohandisiwa zinaweza pia
kudhoofisha ustawi wa mimea ya mwitu na hivyo kuathiri bioanuai. Jaribu
kujiuliza itakuaje jeni mbalimbali zilizopandikizwa katika mimea zitahamia kwa
mimea mwitu mbalimbali.
Watengenezaji wa GMOs wanadai kuwa
muingiliano wa jeni katika mimea umekuwa ukifanyika katika hali ya kawaida siku
zote. Lakini je, imewahi kutokea katika hali ya kawaida bakteria akaingiliana
na mmea (hybridization)? Kwa kuwa teknolojia hii inaweza kuhamisha jeni kutoka
viumbe mbalimbali kama vile bakteria, wadudu na hata wanyama kwenda kwa mimea,
ni dhahiri baada ya muda tutakua na mkanganyiko mkubwa katika vyakula
tunavyokula.
Madhara ya kiafya
Mwaka 2012 mwanasayansi Gilles-Eric
Seralini na wenzake, walichapisha matokeo ya utafiti wao uliochukua miaka
miwili katika jarida maarufu liitwalo ‘The
Journal of Food and Chemical Toxicology’ uliioonesha madhara makubwa ya
matumizi ya vyakula vinavyotokana na mimea iliyohandisiwa jeni pamoja na sumu
ya glyphosate (ambayo ipo katika dawa ya kuulia magugu shambani ya roundup).
Matokeo ya utafiti huo ulioitwa “madhara ya muda mrefu ya roundup na matumizi
ya mahindi yaliyohandisiwa jeni kuhimili roundup”, yalionesha pasi na shaka
kuwa, GMO zina madhara kwa maini na figo pamoja na kusababisha kansa. Kwa
bahati mbaya sana, makampuni ya uhandisi wa kibaiolojia yaliupiga vita utafiti
huu kwa kusaidiwa na serikali za ulaya na hivyo mwaka 2013 ikabidi jarida hili
maarufu liuondoe utafiti huu kwenye chapisho lake.
Ilipofika mwaka Juni 2014, utafiti wa
profesa Seralini na wenzake yalichapishwa tena katika jarida la sayansi ya
mazingira la ulaya (Journal of Environmental Sciences Europe, Volume 26:14). Na
kwa utafiti huo uliofanyika kwa panya imeonesha na kuthibitisha kisayansi
uhusiano mkubwa uliopo kati ya mahindi yaliyohandisiwa jeni pamoja na dawa ya
kuulia magugu ya Roundup, dhidi ya afya ya mifumo ya mamalia. Watafiti hawa
wameonesha pia kuwa, masalia ya sumu ya glyphosate katika mimea inayoliwa
yanauwezo wa kusababisha madhara ya kiafya kwa walaji. (utafiti huu unapatikana
katika wavuti wa http://www.enveurope.com/content/pdf/s12302-014-0014-5.pdf au http://www.enveurope.com/content/26/1/14).
Pamoja na kuwa asilimia kubwa ya mimea
iliyohandisiwa jeni katika nchi ya Marekani (ambapo kwa mwaka 2012, 93% ya soya
na 88% ya mahindi yalikua yamehandisiwa jeni) hutumika zaidi kulisha wanyama,
lakini sumu yoyote iliyoliwa na wanyama hubaki mwilini mwao na kuathiri
maradufu wale watakaokula wanyama hawa. Kanuni hii huitwa biomagnification. Kwa
bahati mbaya mazao yaliyohandisiwa kuhimili dawa za magugu yanapewa uwezo wa
kupokea sumu hiyo bila kudhurika. Hii ina maana kuwa sumu hiyo huendelea kubaki
mwilini mwa mmea, ha hivyo myama yeyote atakayekula mmea huo hula pia na sumu
hiyo, na binadamu anapokula mnyama aliyekula mmea huo nae hupata athari.
Kiwango cha athari hii huendelea kuongezeka kwa kadri mnyororo huu wa lishe
unavyoongezeka (biomagnification).
Moja ya sumu ambayo hutumika katika
madawa ya kuua magugu ni ‘glyphosate’. Utafiti unaonesha sumu hii ina madhara
mengi katika afya ya binadamu. Glyphosate huingilia mfumo wa ‘hormones’ katika
mwili (endocrine disruptor) na hivyo kusababisha matatizo kama kisukari,
ugonjwa wa figo, kupanda kwa pressure ya damu, kuongezeka sana uzito, ugumba,
kupungukiwa nguvu za kiume, kansa (ya matiti, tezi dume, ini, ubongo), ukuaji
nk. Dr Nancy Swanson wa Marekani ameweza kuonesha pia kuwa kuna uhusiano mkubwa
kati ya matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni na magonjwa ya viungo mbalimbali
vya mwili (soma matokeo ya utafiti wa Dr. Swanson katika wavuti wa http://people.csail.mit.edu/seneff/Swanson_et_al_2014.pdf).
Ushahidi zaidi wa madhara ya kiafya
hasa wa sumu ya glyphosate ambayo inatumika katika dawa ya kuuwa magugu ya
Roundup na ambayo huwepo katika mimea iliyohandisiwa jeni ili kutodhurika na
dawa hiyo, umetolewa katika tafiti mbalimbali duniani. Utafiti wa Samsel na
Seneff mwaka 2013, unaonesha wazi jinsi sumu hii inavyoathiri mifumo ya mwili
kwa kuingilia njia za kifiziolojia za vichocheo viitwavyo kwa ujumla Cytochrome
P450 (CYP) pathways. Uharibifu wa vichocheo hivi vinavyohusika pamoja na kazi
nyingine asilimia 75 ya ‘organic
molecules oxidation’, usafirishaji wa madini ya salfa (sulphate transport)
katika majimaji ya damu (serum) na pia utengenezaji wa ‘aromatic amino acid’ katika
bacteria wanaoishi katika utumbo mpana. Kuingilia shughuri hizi za mwili
husababisha madhara ya kiafya baada ya muda mrefu kama vile magonjwa ya mfumo
wa chakula, magonjwa ya moyo, unene, saratani, autism, Alzheimer’s pamoja na
ugumba (soma zaidi utafiti huu katika wavuti wa http://responsibletechnology.org/media/Glyphosate_II_Samsel-Seneff%281%29.pdf). Utafiti wa Kruger 2013, umeonesha
pia glyphosate huua bakteria wenye manufaa katika miili ya farasi na ng’ombe
wakati Shehata na wenzake 2012, waligundua sumu hii huua bakteria wenye manufaa
katika kuku. Kutokuwepo kwa bakteria hawa katika miili ya wanyama husababisha
magonjwa kadhaa katika mfumo wa chakula mfano ‘stomach inflammation.
Tafiti zinazoonesha madhara ya
glyphosate katika miili ya wanyama (mamalia na ndege) zipo nyingi na
zinapatikana kirahisi katika wavuti mbalimbali. Ombi langu ni kuwa, ingawa pia
kuna tafiti zinazoonesha kutokuwapo na madhara ya moja kwa moja ya mimea
iliyohandisiwa jeni kwa afya ya binadamu, lakini kupuuza tafiti za kisayansi
zinazoonesha madhara ya mimea hii itakuwa ni kosa. Tunapaswa kama nchi, na hasa
sisi wananchi ambao ndio tutakuwa wahanga wa madhara ya mimea hii, kuwa na
taarifa sahihi juu ya matumizi ya mimea hii. Hofu yangu kubwa ni kutogeuzwa
majaribio.
JE TANZANIA TUTUMIE GMOs?
Ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo
haya tuyaonayo ya binadamu na ustaarabu wake uliletwa na maendeleo ya kilimo.
Lakini maendeleo yoyote lazima yaongozwe katika muelekeo sahihi hasa katika
kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.
Madhara yanayotajwa na wapinzani wa
mimea iliyohandisiwa jeni yanagusa moja kwa moja uhai wetu kama binadamu na
ustawi wa mazingira yetu. Wale wanaotetea matumizi ya mimea hii mara zote
wamekuwa wakipinga kwa jitihada kubwa mawazo ya wanaopinga GMO. Kwa mfano
wanasema kuwa hakuna madhara ya kiafya kwa binadamu yaliyolipotiwa kuwa
yanatokana na matumizi ya moja kwa moja ya GMOs. Lakini tunaposhughurika na
jambo linalohusu uhai na ustawi wa binadamu, hatuhitaji ushahidi kuwa kitu hiki
kinamadhara, bali kitu kitaruhusiwa kama kuna ushahidi kuwa hakina madhara. Na
hii sio kazi ya walaji kuthibitisha kuwa GMO zina madhara, nadhani ni kazi ya
makampuni haya makubwa kufanya tafiti na wathibitishe kuwa GMO hazina madhara.
Tuzungumzie pia suala nyeti la tatizo
la njaa na utapiamlo. Tatizo hili ndilo limekuwa likitumiwa sana na nchi za magharibi
pamoja na makampuni makubwa duniani ya uhandisi biolojia kuzitaka nchi
zinazoendelea kuanza kutumia mimea iliyohandisiwa jeni. Lakini takwimu za
uzalishaji chakula duniani zinaonesha kuwa dunia haina tatizo la uzalishaji wa
chakula. Chakula kinachozalishwa kwa sasa duniani ni zaidi mara moja na nusu (1
½) ya kiasi kinachotakiwa kuwalisha watu wote duniani. Hiki ni chakula
kinachotosha kulisha watu bilioni kumi (idadi ya watu inayotazamiwa kuwepo
mwaka 2050). Kwa maana hiyo, ni kuwa tatizo la njaa katika nchi zinazoendelea
linatokana na umasikini pamoja na mfumo mbovu wa usambazaji wa chakula. Tatizo sio
uwepo wa chakula, ila ni vipi kinawafikia ambao hawana.
Hitimisho
Kwa mtazamo rahisi ni kuwa, shinikizo
kubwa tunalopewa ili kukubali matumizi ya mimea iliyohandisiwa jeni linasukumwa
zaidi na sababu za kibiashara. Ingawa baadhi ya nchi za kiafrika zimeshakubali
matumizi ya mimea hii, kwa Tanzania na watu wake teknolojia hii inapaswa kupewa
muda zaidi ili tafiti nyingi zaidi zifanyike na hivyo kuthibitisha usalama wa
mimea hii au jinsi ya kupunguza madhara yake. Hii ni kutokana na hali halisi
kuwa, nchi hii ni kati ya nchi chache katika ukanda wa SADC zinazojitosheleza
kwa chakula, kinachotakiwa ni kuelimisha zaidi wananchi ili wapende kula milo
yenye lishe za protein, madini na vitamin pia kama vile mboga za majani, dagaa,
maziwa, maharage (hasa ya soya) na chumvi iliyotiwa madini ya ‘iodine’. Hii
itasaidia kupambana ukali wa janga la utapiamlo.
Mwaka 1998, wanasayansi 24 kutoka
Afrika waliohudhuria mkutano wa umoja wa mataifa waliandika waraka mahususi
uliosema “tunapinga vikali matumizi ya
picha zinazoonesha watoto masikini na wenye njaa wa kiafrika zinazotumika na
makampuni makubwa kusukuma matumizi ya teknolojia ambayo siyo salama, si rafiki
kwa mazingira na isiyokuwa na faida za kiuchumi kwetu. Hatuamini kama
teknolojia ya uhandisi jeni kama itasaidia wakulima wetu kuzalisha chakula
kinachohitajika katika karne ya 21. Badala yake tunafikiri teknolojia hii itaharibu
mazingira, elimu yetu ya asili na mfumo endelevu wa kilimo ambao wakulima wetu
wameuendeleza kwa milenia kadhaa na kwamba teknolojia hii itadumaza uwezo wetu
wa kujitengenezea chakula”
Kama malengo ya makubaliano ya
Cartagena (Cartagena Protocol on Biosafety) ya mwaka 2003, ni jukumu la kila
nchi hasa zinazoendelea kutengeneza sera madhubuti zitakazolinda mifumo yetu ya
asili ya ukulima dhidi ya matumizi ambayo usalama wake unatiliwa shaka. Hivi
inawezekanaje watu wanje ya Afrika walio maelfu ya kilometa kutoka kwenye
mashamba yetu wakajua zaidi kuhusu kilimo chetu kuliko sisi? Au ndo tukumbuke
ule usemi wa Dwight D. Eisenhower aliyesema “ukulima ni mwepesi sana kama jembe lako ni kalamu na umekaa maili
nyingi kutoka shambani”
Mwandishi
wa Makala hii ni mwajiriwa wa idara ya biolojia katika chuo kikuu cha
kikatoliki Mwenge, Moshi-Tanzania. Kwa sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili
katika sayansi ya mimea katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Ni mkereketwa wa
mazingira asili.
No comments:
Post a Comment